Mbogamboga

Kifahamu Kilimo cha Zao La Beetroot (Kiazi Sukari)

By  | 

Beetroot ni moja kati ya Mazao yatokanayo na Mizizi kama Vile Viazi Ulaya, Viazi vitamu na aina nyingine ya mazao yafananayo na mazoa tajwa hapo. Kitaalamu Beetroot inajulikana Kama Beta vulgaris

Beetroot ni muhimu sana kwa kuongeza damu na kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali. Inaweza kuliwa kama ilivyo baada ya kuvunwa au ikatengenezwa juice na ikatumika vizuri kabisa.

Lakini  pia majani yake yanalika kama spinach. Kwa ukuaji bora wa mimea hii inahitaji mvua ya kutosha. Pia hukubali vyema katika udongo wenye rutuba na wa kitifutifu. Udongo wa mfinyanzi ambao ukikauka unapasuka husababisha tunda kuwa na umbo ambalo sio zuri kibiashara.

Kilimo cha Zao La Beetroot

AINA ZA BITIRUTI (BEETROOT)

Kuna aina mbalimbali za bitiruti kama vile vyekundu vyenye mistari myeupe kwa ndani, pamoja na nyeupe, hata hivyo bitiruti ndiyo inayolimwa kwa wingi nchini kwetu Tanzania.  Aina zote hizi huweza kuliwa majani na mizizi pia.  Hata hivyo kutokana na kiwango cha sukari inayopatikana, huwa na ladha zaidi kama kikiliwa kibichi.

MATUMIZI

Zao hili lenye madini ya foliate, chuma, magnesiamu, vitamin C na potashiamu lina matumizi mengi kwa binaadamu na hata kwa wanyama.
 • Bitiruti hutumika kama chakula au kiungo kama vile karoti kwa ajili ya kuongeza ladha kwenye vyakula mbalimbali.
 • Zao hili hutumika kutengenezea juisi.  unaweza kutumia bitiruti pekee au ukachanganya na matunda mengine.
 • Huongeza damu mwilini pamoja na kuupa mwili nguvu na kusaidia kuboresha kumbukumbu.
 • pia inasadikiwa hutibu ugonjwa wa sukari, kuvimbiwa, majeraha na magonjwa ya ngozi.
 • Zao hili pia majani yake huweza kutumiwa kama lishe kwa ajili ya kulishia mifugo wa aina yoyote.

MAHITAJI YA UDONGO

Zao hili husawi zaidi katika udongo wenye uchachu uchachu (soil ph) kuanzia 5.8-8.0 na kama udongo utakuwa haujapimwa ni bora mkulima akapima ili ajue kwa kuwa kama udongo una asidi nyingi utaathiri sana ukuaji wa zao hili kwa kusababisha upungufu wa virutubisho muhimu.

KUANDAA SHAMBA

Mbegu huoteshwa shambani kabisa wala hamna haja ya kusia mbegu. Hivyo hapa nakushauri ndugu mkulima ulime vizuri kwa kuondoa majani, visiki, na takataka zoote na utifue vizuri kina cha sm 15-20, vunja vunja kasha sawazisha shamba lako. Baada ya hapo nyanyua matuta juu ili kuweka mzunguko mzuri wa hewa na pia njia nzuri ya usafirishaji maji. Udongo uondolewe uchafu woote ikiwemo mimea iliyooza.

KUOTESHA NA NAFASI ZA KUOTESHA

Mara baada ya kuandaa shamba, utachukua mbolea ya samadi ambayo  utaichanganya na udongo wakati wa kunyanyua matuta yako. Kisha baada ya hapo mbegu inapaswa kuoteshwa chini kwenye kina cha sm 1 hadi 2.5 kwenda chini. Kasha mkulima aandae tuta lenye urefu apendao yeye na upana wa mita moja.

Kisha mkulima anaweza kuandaa mstari mmoja akaupanda beetroot zikaachana sm 10, kasha mstari kwa mstari zikaachana sm 20-45. Au

Aweke vijimstari viwili ndani ya tuta moja au vijimstari viatatu ndani ya tuta moja. Nfasi ya mche kwa mche iwe sm 10, mstari kwa mstari kwa mstari sm 20. Na tuta kwa tuta anaweza akaacha hata mita moja. Angalia aina tofauti tofauti za uoteshaji chini.

Mara baada ya kuchimba vijimstari na aoteshe huko mbegu za beetroot kisha afukie na udongo kidogo tena mwepesi ili kurahisisha mbegu kuota. Mara baada ya kuotesha aweke matandazo makavu kisha aanze kumwagilia maji asubuh na jioni baada ya siku 5-12 mbegu zitakuwa zishaanza kuota.

UWEKAJI WA MBOLEA

Uwekaji wa mbolea mara kwa mara ni jambo muhimu mno. Nikiwa na maana kiwango cha naitrojeni kinachowekwa udongoni, fosiforasi na potash kiwekwe mara kwa mara yaani kwa mbolea za dukani ni sawa na kusema uwekaji wa NPK. Ila uwekaji wa mbolea ni vizuri ukatokana na vipimo. Majibu yanasemaje kuhusu kuwepo kwa virutubisho hivyo muhimu vitatu kwenye udongo wako? Kisha sasa anza kuweka mbolea. Mara nyingi huwa namshauri mkulima awe anaweka mbolea asili ya ng’ombe. Ikiwezekana kila baada ya siku saba. Unachukua mbolea ya ng’ombe iliyooza vizuri unarushia katika mimea yako kisha unamwagilia maji.

KUMWAGILIA MIMEA MAJI

Baada ya miche kuchipua, anza kumwagilia katika wiki ya pili. Mwagilia kila wiki mara moja au mbili kulingana na ukavu wa shamba. Zao hili halihitaji maji mengi kwani husababisha fangasi pamoja na kuoza kwa kiazi hivyo usimwagilie kila wakati.

MAGONJWA NA WADUDU

WADUDU

APHIDS

Wadudu hawa huwa na rangi tofauti tofauti mfano kuna ambao huwa na rangi ya dark brown na wengine huwa na rangi ya kijani (green), urefu wao huwa mm 2 na hupendelea kukaa chini ya majani na kufyonza tishu za mmea huko na wanapokuwa wengi hupelekea jani kujikunja na kusinyaa.

KINGA

Tafuta dawa iitwayo ATTAKAN C, ABAMECTING, DUDU ALL na nyinginezo za wadudu. Lakini pia kulima mazao ya mzunguko husaidia pia kupunguza wadudu hawa kwani itawafanya wasiyazoee mazingira ya shambani. Dawa hizi pia zitasaidia kuuwa wadudu wakatao majani.

MABAKA MEUSI

Huu ugonjwa huletwa na fangasi ambaye huingia katika majani na kusababisha mabaka. Mabaka haya huwa na kipenyo cha kuanzia mm 3 na huanza na rangi ya brown na baadae kuwa na rangi ya grey. Mara nyingine hutokea katika mauwa.

KINGA

 • Kinga mbegu yako na madawa ukishaotesha mfano
 • Fanya kilimo cha mzunguko
  Epuka kutoamisha maji

UBWIRU CHINI (DOWNY MILDEW)

Dalili za ugonjwa huu ni pale ambapo jani litabadilika rangi na kuwa wa njano kisha baadae kuwa la brown kabisa. Lakini pia rangi ya grey yaweza kuonekana chini ya jani la mmea.

GAMBA LA JANI

Kwa maeneo ambayo udongo wao utakuwa na asidi nyingi. Majani huweza kuathirika na ugonjwa huu. Pale ambapo jani litetengeneza kitu kama gamba gumu hivi.

KINGA

Kinga ni kupima udongo kujua kiasi cha asidi kasha kupata ushauri juu ya hilo

KUTU YA MMEA

Hapa mmea huwa na vidoa vidogo vidogo sana ambavyo vina rangi ya machungwa au red brown.Ugonjwa huu mara nyingi hauna madhara makubwa kama mmea umeshaweka tunda.

KUOZA MZIZI NA KATA KIUNO (ROOT ROT AND DAMPING OFF)

Magonjwa haya hutokea sana katika maeneo yenye udongo mgumu unaokakamaa hasa udongo wa mfinyanzi. Hivyo hata mbegu uotaji wake huwa wa shida sana. Mbegu huanza kuota ikiwa na afya ambayo sio nzuri, mmea ukiwa mdogo waweza badilika rangi ukawa wa njano, ukasinyaa, kujikunja, mizizi kuwa na rangi nyeusi. Lakini pia kukata kiuno kwa mmea huweza tokea mmea ukiwa mdogo pale ambapo maji yatakuwa yakimwagiliwa bila kufuata mtiririko maalumu. Hii ikapelekea kutoamisha maji na hapo kupelekea mmea kujikunja na kuanguka.

KINGA

 • Mbegu ioteshwe katika udongo mlaini uliotifuliwa vizuri
 • Inunuliwe mbegu kwa wauzaji wa kuaminika mara nyingi mbegu iwe inalindwa na thiram.
 • Kufanya kilimo cha mzunguko
  Super grow au Mult k itumike kuongeza virutubisho kama boron kwa mmmea
 • Mbegu isioteshe zaidi ya sm 2.5 kwenda chini
 • Epuka kutoamisha maji na uwe na ratiba maalumu ya umwagiliaji.

MAVUNO

Zao hili hukomaa na kuvunwa baada ya miezi mitatu (siku 90).  Hata hivyo huweza kuvumilia kusubiri soko ikiwa mkulima atalazimika kufanya hivyo (huweza kukaa miezi mitatu toka kukomaa bila kuharibika kwa kuvuna na kuhifadhi sehemu yenye ubaridi kiasi).
 USHAURI
 Kutokana na matumizi ya zao hili, si vyema kutumia kemikali.  Ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo hai ili kulinda afya za walaji.

Ukiniita Mtokambali bado utakua sahihi, karibu na Hili ndilo chimbo langu, Utajifunza Mengi yahusianayo na Kilimo. Kwa pamoja tuikuze mtokambali.com. Ungana nami twitter@mawere3. Siku zote "Haja ya Mja hunena na Uungwana ni vitendo"

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *