Matunda

Yajue Maandalizi ya Kilimo cha Papai, Kuandaa kitalu na mbegu

By  | 

Mambo muhimu yakuzingatia katika kilimo cha papai ni pamoja na kuwa na chanzo chakuaminika cha maji kwa ajili ya Umwagiliaji katika kitalu chako, na ni vizuri pia kitalu hicho kiwe karibu na nyumbani kwako ili uweze kukihudumia kwa wakati. Hakikisha pia kitalu chako kina uzito au usalama wakutosha ili kuzuia wezi na wanyama waharibifu.

Unapokuwa na Uhakika wa mambo hayo hapo juu, sasa andaa Mbolea ya samadi iliyooza kwa muda mrefu,utakayoichanganya na udongo, andaa pia pumba za mpunga na vumbi la Mkaa na kuyachanganya na udongo, andaa pia majani ya mwarobaini kisha yapondeponde/kusaga.

Maandalizi hayo yafanyike kwa vipimo kama ifuatavyo;

Kwa mfano, ukichukua udongo wako ndoo moja kubwa, changanya na Molea ndoo ndogo moja, sadolini moja ya pumba na vumbi la mkaa kisadolini kimoja na majani ya Mwarobaini nusu Kisado.

Ukisha changanya udongo na pumba, unashauriwa kuupika udongo huo(Kitaalamu tunaita Sterilization,) kisha sasa changanya na mwarobaini pamoja na Vumbi la Mkaa. Mwarubaini hapa unatumika kama njia moja wapo za asili inayotumika kuua wadudu waharibifu.

Jinsi ya Kupika Udongo.

Unatakiwa uwe na vifaa kama Karai, au chombo cha shaba, moto, ndoo yenye maji, kipande cha Bati kwa ajili kwa ajili ya kumwaga udongo wako uliopikwa.

Hakikisha udongo wako unakua umeunyunyuzia maji kidogo(Unyevu) Kisha Funika chombo chako ili upate mvuke. Geuza udongo wako mara kwa mara huku ukichochea moto. Utabaini kuwa udongo wako upo teyari kwa njia hizi tatu ambazo moja ni udongo kutoa harufu ya kuungua, ya pili ni udongo kutoa mvuke na ya tatu ni kuupika udongo kwa muda wa saa moja.

Unashauriwa udongo unaoutumia uwe ni ule wa msituni kwakua haujawahi kulimwa, hivyo una virutumisho vya Kutosha. Ukisha epua udongo, Umwage katika chombo cha bati kisha uache kwa masaa 12 hadi 24 kabla ya  kuanza kwa zoezi la Kuuweka kwenye Viroba.

Jaza vizuri udongo kwenye kiriba na na usiache nafasi ya Hewa, unaweza kuunyunyuzia udongo huo maji ili ushikamane vizuri. Baada ya hapo, pulizia dawa ya kuuwa wadudu kama vile Rapid Attack, Confidor na nyinginezo. Baada ya siku moja ama mbili ya kuweka dawa, sasa unaweza kupanda mbegu zako, huku ukihakikisha viriba vyako vipo sehemu yenye mwanga wakutosha. Andaa pia nyasi kavu laini kwa ajili ya matandazo baada ya kuweka mbegu kwenye viriba.

Maandalizi ya Mbegu.

Unatakiwa uwe makini katika manunuzi ya mbegu hasa kwa mtu anayetaka kuanzisha kilimo hichi kwa minajili ya Bishara. Itakubidi utafute wataalamu ili waweze kukushauri juu ya mbegu bora. Ukishanunua mbegu bora ulizoridhika nazo kutokana na maelezo ya wataalmu, loweka mbegu hizo kwa maji masafi na chombo kisafi kwa muda wa siku 2 hadi 3 na kila baada ya masaa 6 hadi 8 badili maji hayo.

Ukiona mbegu inaelea juu basi tambambua kwa mbegu hiyo haina uwezo wa kuota hivyo unashauriwa kuitoa. Baada ya siku hizo, funga mbegu zako kwenye mfuko mweusi kisha weka kama mbegu chache chache kama mia hadi 20 kwa kila mfuko, mfuko huo ufungwe vizuri na usiruhusu hewa kupita kisha hifadhi sehemu nzuri na safi.

Uache mfuko kwa muda wa siku tano hadi saba, kisha ufungue na ukague kama mbegu zako zimeanza kutoa mikia yenye rangi nyeupe. Zilizotoa mikia ni dalili kuwa ziko teyari kwa ajili ya kupandwa na ambazo bado, Endelea kuziacha kwenye mfuko.

Wakati wa Kusia mbegu kwenye viriba, hakikisha udongo una unyevu kisha weka mbegu katika tobo lenye urefu wa sentimita moja na siyo zaidi ya hapo. Baada ya kusia mbegu zako, tandika nyasi kavu juu kwa lengo la kutunza unyevu katika udongo ule na kuzuia mwanga wa jua moja kwa moja. Baada ya kutandika nyasi, pulizia dawa tena mfano Confidor ili kuua wadudu walioko kwenye nyasi.

Funika nyasi kwa siku 5 hadi 7, kisha mbegu zako utakuta zimeota. Zikishaota, ondoa nyasi. Kitaalamu kitalu cha mipapai kinakaa kwa muda wa siku  35 hadi 40 chini ya uangalizi maalumu wa kitaalamu. Kwa kipindi chote hicho, mwagilia maji na kagua miche yako kila mara ili kukagua magonjwa kama vile fangus. Ikifika siku 30, punguza umwagiliaji maana tunaanda miche kuwa teyari kuzoea shida na kwenda shamba kubwa.

Mmea ukifikisha sentimita 15-20 utakua teyari kwenda shambani.

 

Credit to: Jackson Bwire 0715500136

Ukiniita Mtokambali bado utakua sahihi, karibu na Hili ndilo chimbo langu, Utajifunza Mengi yahusianayo na Kilimo. Kwa pamoja tuikuze mtokambali.com. Ungana nami twitter@mawere3. Siku zote "Haja ya Mja hunena na Uungwana ni vitendo"

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *